Nchi Wanachama Wa SADC Kuimarisha Sera Na Kujenga Mikakati Ya Pamoja Ya Kukuza Ajira Kwa Vijana
Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
(SADC) zimejizatiti kuimarisha Sera na kujenga mipango ya pamoja itakayowezesha
kukuza ajira kwa vijana katika Ukanda huo.
Akifungua Mkutano wa Makatibu Wakuu, Maafisa Waandamizi na
Wadau wa Utatu wa Jumuiya hiyo wanaosimamia Sekta ya Kazi na Ajira hii leo
Machi 2, 2020 Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana,
Ajira na Wenye Ulemavu Bw. Andrew Massawe alisema kuwa Mkutano huo
umewakutanisha Wataalamu wa sekta ya Kazi na Ajira kwa lengo la kuandaa nyaraka
mbalimbali zitakazo jadiliwa katika Mkutano wa Mawaziri ambao utafunguliwa
rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu
Hassan tarehe 5 hadi 6 Machi, 2020 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius
Nyerere.
Alieleza kuwa ajenda zitakazo jadiliwa ni pamoja na masuala
ya kisera kuhusu ukuzaji wa ajira kwa vijana, pia masuala yanayohusisha uhamaji
wa nguvu kazi ndani ya jumuiya ya SADC ambapo itasaidia pia kutoa fursa ya
kukuza ajira kwa nguvukazi ya nchi wanachama.
“Itambulike kuwa uimarishwaji wa sera katika sekta ya kazi
na ajira utasaidia kwa kasi kikubwa kuwa chachu ya maendeleo ya nchi wanachama
wa Jumuiya ya maendeleo kusini mwa afrika endapo itasimamiwa vizuri,” Alisema
Massawe
Aliongeza kuwa kauli mbiu ya Mkutano huo isemayo “Kukuza
Soko la Ajira na Mahusiano Mema Sehemu za Kazi kwa Maendeleo Endelevu”
inaelezea umuhimu wa sekta ya kazi na ajira katika kuongeza tija ya ukuaji wa
soko la ajira kwa nchi wanachama.
Naye Naibu Katibu Mtendaji mwenye dhamana ya Utangamano wa
Kikanda, Dkt. Thembinkosi Mhlongo alieleza kuwa mapendekezo yaliyotolewa katika
mkutano uliofanyika mwezi Novemba 20, 2019 ulioshirikisha wataalamu na wadau wa
utatu umechangia katika kujenga miongozo sahihi na sera zitakazo wawezesha nchi
wanachama wa SADC kukuza sekta ya kazi na ajira.
Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Ajira na Ukuzaji Ujuzi, Bw.
Ally Msaki alisema kuwa Mkutano wa Mawaziri utakao funguliwa rasmi tarehe 5
Machi, 2020 utawawezesha Mawaziri wa Nchi wanachama wa SADC kujadili kwa pamoja
ajenda mbalimbali zitakazokuwa zimepitiwa kwenye kikao cha wataalam kwa lengo
la kuimarisha sekta ya kazi na ajira nchini na jumuiya hiyo kwa ujumla.
Hadi sasa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa
Afrika (SADC) zilizoshiriki katika Mkutano huo ni Angola, Afrika Kusini,
Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Msumbiji, Zambia, Zimbabwe, Malawi,
Namibia, Eswatini, Lesotho, Jamhuri ya Shelisheli na Tanzania.
MWISHO

Comments
Post a Comment