Sekretarieti Ya Ajira Yatakiwa Kutenda Haki Ili Kuiwezesha Serikali Kupata Watumishi Wenye Sifa Stahiki
Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary
Mwanjelwa (Mb) wakati akizungumza na watumishi wa Sekretarieti ya Ajira katika
Utumishi wa Umma alipofanya ziara ya kikazi katika ofisi hiyo iliyopo Magogoni
jijini Dar es Salaam, yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji, kufahamu kwa kina
majukumu ya Sekretarieti hiyo na kujiridhisha namna Sekretarieti hiyo
inavyotekeleza majukumu yake ya kila siku.
Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesema kuwa, Sekretarieti ya Ajira
katika Utumishi wa Umma ni chombo ambacho kinatakiwa kutenda haki ili Serikali
ya Awamu ya Tano ipate watumishi wenye sifa na vigezo watakaoendana na kasi ya
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ya
kuliletea taifa maendeleo katika sekta za miundombinu, afya, viwanda, biashara,
kilimo, usafiri wa anga, elimu na uchumi
kwa ujumla wake.
Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesema kuwa, awali Sekretarieti ya
Ajira katika Utumishi wa Umma ilikuwa ikilalamikiwa sana kuwa, mchakato wa
kuomba kazi Serikalini ulikuwa ukichukua muda mrefu kiasi cha waombaji kusahau
kama waliwasilisha maombi, hivyo ameipongeza Sekretarieti kwa kubuni mfumo wa
upokeaji wa maombi ya kazi (Recruitment Portal) na mfumo wa kupanga wasailiwa
waliofaulu ambayo kwa kiasi kikubwa imepunguza malalamiko yaliyokuwa yakitolewa
na waombaji wa ajira Serikalini na kuongeza kuwa, hivi sasa mchakato wa ajira
mpya unachukua siku 52 tu licha ya kuwepo taratibu nyingi zinazozingatiwa
kukamilisha mchakato mzima.
Mhe. Dkt. Mwanjelwa amefafanua kuwa, mfumo huo una kanzi
data ya waombaji wote waliofanyiwa usaili na kupata ufaulu mzuri lakini kutokana
na uwepo wa fursa chache za ajira hawakupangiwa vituo vya kazi, hivyo
unaiwezesha serikali kupata watumishi kwa wakati pindi wanapohitajika haraka
katika Taasisi za Umma.
Sanjari na hayo, Mhe. Dkt. Mwanjelwa ameitaka Sekretarieti
ya Ajira katika Utumishi wa Umma kutobweteka kwa mafanikio waliyoyapata kupitia
mfumo wa Ajira Portal na badala yake waongeze kasi ya ubunifu ili kuendana na
kasi ya mabadiliko ya Serikali ya Awamu ya Tano ambayo imedhamiria kwa dhati
kuboresha huduma zinazotolewa na Taasisi za Umma nchini.
Kwa upande wake, Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika
Utumishi wa Umma, Bw. Xavier M. Daudi, amesema ofisi yake ilianzishwa kwa lengo
mahususi la kukabiliana na changamoto za ajira zilizokuwa zikijitokeza hapo
awali, hivyo iliundwa ili kuongeza uwazi, kutenda haki na kuhakikisha kuwa
ajira zinapatikana kwa kuzingatia sifa.
Bw. Daudi amesisitiza kuwa, ofisi yake kwa kushirikiana na
waajiri inazingatia Sera ya Ajira, Sheria, Kanuni na Taratibu katika kusimamia
mchakato wa ajira katika Utumishi wa Umma kwa lengo la kuiwezesha Serikali
kupata watumishi wenye sifa na maadili mema watakaoisaidia Serikali kufikia
malengo yake makubwa iliyojiwekea, ikizingatiwa kuwa watumishi ndio injini ya
utekelezaji wa majukumu ya Serikali.
Naye, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Sekretarieti ya Ajira
katika Utumishi wa Umma, Bw. Mbarak Abdulwakil amemshukuru Mhe. Dkt. Mwanjelwa
kwa nasaha zake za kuitaka Sekretarieti kuzingatia weledi katika jukumu zito la
kuwezesha ajira za watumishi wa umma na kumhakikishia kuwa, maelekezo yote aliyoyatoa yatatekelezwa kikamilifu na
Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.
Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma inatekeleza majukumu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kutafuta wataalam wenye ujuzi maalum na kuandaa mfumo wa kuifadhi taarifa za wataalam, kutangaza nafasi wazi za kazi zinazojitokeza katika Utumishi wa Umma, kuhusisha wataalam ili kushirikiana nao kwa ajili ya kufanya usaili kulingana na mahitaji, kuwashauri waajiri kuhusu masuala mbalimbali yanayohusiana na mchakato wa ajira, kuandaa orodha ya wahitimu wa vyuo na wataalam kwa weledi kwa madhumuni ya kurahisisha rejea za ujazaji nafasi na kuendesha mchakato wa ajira wa Watendaji Wakuu wa Wakala na Idara zinazojitegemea za Serikali.

Comments
Post a Comment